Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala nchini Tanzania (KIUT), Profesa Tolly Mbwette amesema licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kuhusu elimu, bado inatakiwa kuangalia ubora wa elimu inayotolewa.
Amesema mataifa mbalimbali duniani yana maazimio kuhusu ubora wa elimu ili kuhakikisha inayotolewa hasa katika vyuo vikuu inakuwa na manufaa kwa wanafunzi na Taifa.
Ameeleza hayo leo Jumatano Desemba 11, 2019 katika kongamano la kwanza lililoandaliwa na chuo hicho.
Profesa Mbwette amesema lengo la kuanzisha kongamano hilo ni kujadili na kuhakikisha nchi inakuwa na wasomi wenye uwezo wa kutumia elimu yao kuliwezesha Taifa kusonga mbele.
“Kwa hiyo nimeagiza walimu, wafanyakazi, wanafunzi wa sasa na waliomaliza kuhakikisha wanashirikiana pamoja kutatua changamoto za elimu ikiwemo kuweka mazingira wezeshi ya kujisomea na hili suala la elimu bora iwe utamaduni wetu.”
“Leo tunajadili suala hili lakini halitoishia hapa tunataka ifikapo 2030 linakuwa mtambuka na linatumika kama yanavyofanya mataifa mengine,” amesema.
Amesema ajenda ya elimu bora inalenga kuangalia aina ya elimu anayopatiwa mwanafunzi ambayo inampatia maarifa sio tu ya kuajiriwa bali kujiajiri mwenyewe.
Mmoja ya wanafunzi waliowahi kusoma chuoni hapo, Rashid Shangazi amesema kongamano hilo litakuja na mapendekezo mbalimbali na kutatua changamoto chuoni hapo.
Shangazi ambaye mbunge wa Mlalo (CCM) amesema kinachoshusha ubora wa elimu katika vyuo ni sera.