Kipigo cha mabao 2-0, ilichokipata timu ya soka ya Chuo cha Kimataifa cha Kampala nchini Tanzania (KIUT), dhidi ya Guardian Angels ya Kigamboni, kimempa funzo kocha Erius Marius.
KIUT ilipoteza mchezo huo dhidi ya Guardian Angels, katika mechi ua kirafiki iliyochezwa juzi, Uwanja wa KIUT, uliopo Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini na gazeti hili, baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Marius alisema amepata funzo kupitia mechi hiyo, hivyo anakwenda katika uwanja wa mazoezi kuhakikisha anarekebisha makosa yaliyojitokeza.
Alisisitiza kuwa kilichomponza katika mechi hiyo ni kipindi cha kwanza kupanga wachezaji wengi wa kikosi cha tatu, ambao walionesha kiwango cha chini hatimaye kuruhusu mabao hayo.
“Nilianzisha kikosi changu cha tatu ndiyo maana uliona mabao yote mawili tulifungwa kipindi cha kwanza na nilipofanya mabadiliko ya kikosi kipindi cha pili hakukuwa na bao lililoingia,” alisema.
Marius alisema kutokana na matokeo hayo, ameanza kukiboresha kikosi hicho hususani katika maeneo ya ulinzi na kiungo kuhakikisha kinakuwa bora zaidi.
Chanzo:
Mwandishi: SIMON NYALOBI
Chombo Habari: GAZETI LA UHURU
Tarehe: JUMATANO JUNI 4, 2025