Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala Tanzania (KIUT) kimepata heshima ya kipekee baada ya baadhi ya wanafunzi wake kuchaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika Mashindano ya Mpira wa Wavu wa Ufukweni (National Tour) yanayotarajiwa kufanyika Wilaya ya Rubavu, nchini Rwanda kuanzia Juni 13 hadi 15, 2025.
Msafara wa watu 12, wakiwemo wachezaji wanane na viongozi wanne, uliondoka nchini Jumatano, Juni 11, kuelekea Rwanda kushiriki mashindano hayo ya kimataifa. Ushiriki huu ni sehemu ya juhudi za kuendeleza vipaji vya michezo miongoni mwa vijana wa Kitanzania.
Safari hiyo imeandaliwa na Faru Sports Foundation kwa kushirikiana na Sand für Alle, taasisi ya michezo kutoka Ujerumani, ikiwa na lengo la kuwapa vijana fursa ya kushiriki mashindano ya ngazi ya juu na kupata uzoefu wa kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Faru Sports Foundation, Robin Msigwa, amesema mashindano hayo yamejumuisha wachezaji kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani, ikiwa ni pamoja na vyuo na klabu huru.
“Ushiriki wa mashindano haya si tu fursa kwa vijana kuonyesha uwezo wao, bali pia ni maandalizi muhimu kuelekea mashindano mengine ya ndani na nje ya nchi,” amesema Msigwa.
Msigwa ameongeza kuwa wachezaji wanaoshiriki wanatoka katika taasisi na maeneo tofauti nchini, yakiwemo Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala Tanzania (KIUT), TAI, na Zanzibar.
Kwa upande wa KIUT, chuo hicho kimeelezea fahari yake kwa kuona wanafunzi wake wakichaguliwa kuiwakilisha nchi, hali inayoonyesha mchango wa taasisi hiyo katika kukuza vipaji vya michezo nchini.
“Huu ni ushahidi kuwa taasisi za elimu ya juu nchini zinatoa mchango halisi katika kukuza michezo na kutoa fursa za kimataifa kwa vijana wetu,” amesema msemaji wa KIUT.
Mashindano haya yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa wachezaji kuonyesha uwezo wao, kujiandaa kwa mashindano yajayo na kujenga uhusiano wa kimichezo wa kimataifa.