Muktasari:
Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi amewaasa wahitimu wa chuo kikuu cha kimataifa cha Kampala Tanzania (KIUT), kuwa ujuzi na maarifa waliyoyapata wakatumie kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Dar es Salaam.
Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi amewaasa wahitimu wa Chuo Kikuu cha kimataifa cha Kampala Tanzania (KIUT), kuwa ujuzi na maarifa waliyoyapata wakatumie kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza jana Desemba 17 katika mahafali yaliyofanyika chuoni hapo Gongolamboto jijini hapa, Mwinyi maarufu kwa jina la Mzee Ruksa, amesema anaamini wahitimu kutoka chuo hicho wamepata elimu itakayo kwenda kubadilisha jamii zao na kuendeleza uchumi wa taifa.
Jamii inatarajia ya kwamba sasa mna upeo wa hali ya juu katika kupambana na changamoto zinazokwamisha maendeleo, amesema.
Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha Mzee Ruksa, Makamu mkuu wa chuo hiko, Profesa Angwara Kiwara amewaasa wahitimu hao, kutokutegemea ajira za Serikali pekee, badala yake wawe wafanisi katika kuanzisha biashara zao.
Chuo chetu kinatoa kozi ya ujasiriamali hivyo ni imani yangu somo hili walilizingatia vyema na watakwenda kutumia maarifa waliyo yapata, amesema.
Mmoja wa wahitimu hao, Euzebyo Msigwa ambaye alipewa tuzo ya mwanafunzi bora katika fani ya utawala kwa umma, amesema ushirikiano baina yake na wanafunzi wenzake ndio siri ya mafanikio yake.
Huwezi kufaulu bila kuwa na malengo, katika elimu mwanafunzi anatakiwa ajiwekee malengo bora yatakayo mtambulisha katika jamii katika siku zijazo amesema Msigwa.
Naye mwanafunzi bora katika fani ya benki na fedha, Sabah Suleimani mwenye ufauli wa GPA ya 4.6 amesema siri ya mafanikio yake ni kusoma kwa bidii heshima kwa walimu na kutokumdharau mtu yeyote.
Mwanafunzi bora fani ya Benki na Fedha Chuo Kikuu cha kimataifa cha Kampala Tanzania (KIUT), Sabah Suleimani. Picha Emmanuel Msabaha
Nawaasa wanafunzi ambao bado wanaendelea na masomo, kujiamini na kuamini kile
wanachokifanya ni bora huku wakifata ushauri wa waalimu wao, amesema Sabah.
Chanzo:
Emmanuel Msabaha, Tarehe 18 Desemba 2022, Gazeti ya Mwananchi
Tovuti ya Habari:
Mzee Mwinyi awataka wahitimu KIUT kutatua kero za jamii | Mwananchi