Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amewahimiza wahitimu kutoridhika na kiwango cha elimu walichofikia.
Dar es Salaam. Wahitimu wamehimizwa kutumia elimu na maarifa waliyopata chuoni kwa vitendo, wakihakikisha wanasaidia kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Hayo yameelezwa leo Desemba 12, 2024 na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala nchini Tanzania (KIUT), Profesa Peter Msola katika mahafali ya saba ya chuo hicho.
Profesa Msola amesema jamii inatarajia wahitimu wamepata elimu ambayo imeongeza kwa kiasi kikubwa upeo wao katika kufanikisha upatikanaji wa maendeleo.
Amesema dhima kuu ya kuwekeza katika elimu popote ni kuisaidia jamii kutatua changamoto inazokabiliana nazo.
“Kwa hakika uthibitisho mkubwa wa maarifa na ujuzi wenu mlioupata utathibitika kutokana na utendaji kazi wenu huko mwendako, nendeni mkawe mabalozi wazuri na kuzingatia kile mlichofundishwa,” anasema.
Pia amewasisitiza kutumia maarifa waliyopata kujiajiri na kutengeneza fursa kwa wengine.
Amewataka kuwa wepesi wa kuangalia sehemu nyingine ambazo maarifa na ujuzi wao unaweza kutumika kwa ufanisi zaidi kuliko kusubiri ajira serikalini au katika sekta binafsi.
“Muwe watu wa kutafuta fursa badala ya kusubiri fursa ziwafuate jambo ambalo si rahisi kutokea katika dunia ya leo ambayo ni kijiji chenye ushindani mkubwa,” amesema.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amewahimiza wahitimu kutoridhika na kiwango cha elimu walichofikia, akieleza huo ni mwanzo tu wa maisha ya taaluma.
Amesema kufikia hatua hiyo ni moja kati ya hatua za kuzifikia ndoto zao, hivyo ni vyema kuliangalia suala la kujiendeleza kitaaluma kwa umakini.
“Leo mnafurahi na kusheherekea mahafali haya lakini haimaanishi ndiyo mwisho wa kusoma, safari bado ni ndefu kama wasemavyo Waswahili elimu haina mwisho,” anasema.
Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Profesa Yunus Mgaya amewakumbusha wahitimu ili waweze kuisaidia jamii kutatua changamoto zinazowazunguka sharti kujiamini, kujitambua, kuweka malengo na kuyasimamia kikamilifu.
“Elimu mliyoipata si yenu pekee bali ni manufaa ya jamii inayowazunguka,” amesema.
Chanzo: Mariam Mbwana – Mwananchi Communications Ltd
Tarehe: Alhamisi, Desemba 12, 2024